Mwezi mkubwa zaidi kuonekana duniani
MWEZI mpevu utakaoonekana leo Novemba 14, siyo tu ni mwezi
mpevu ulio karibu zaidi na Dunia mwaka huu, bali pia ni mwezi mpevu ulio
karibu zaidi katika karne hii ya 21.Hali ya mwezi mpevu kukaribia zaidi na dunia katika kipindi
cha mwaka wowote ndicho kinajulikana kama Mwezi Mpevu Ajabu (Super
Moon) na hii kwa sababu unaonekana mkubwa zaidi kuliko ule unaoonekana
unapokuwa mbali zaidi kutoka duniani.Kwa jina la kitaalamu Mwezi Mpevu Ajabu huitwa pia
perigee-syzygy. Kila mwaka kuna Mwezi Mpevu Ajabu, lakini huu wa leo ni
wa ajabu kwa sababu ni wa karibu zaidi katika miaka 67 iliyopita tangu
mwaka 1948, na hautakuwa karibu kiasi hiki tena kwa miaka 18 ijayo hadi
Novemba 25, 2034.Kitu chochote kikiwa mbali nasi, huonekana kidogo na kikiwa
karibu kinaonekana kikubwa. Hali hii hutokea kwa mwezi pia, kwa vile
mzingo wa mwezi kuizunguka dunia si duara kamili ila ni umbo la
mduaradufu au mduara mithili ya yai.
Kwa hiyo kila mwezi umbali wake na dunia hubadilika kutoka
juu zaidi hadi chini zaidi. Ukubwa wa mwezi tunavyouona kutoka hapa
duniani hubadilika kutegemeana na umbali wake kutoka ardhini. Wastani wa
umbali kutoka Duniani mpaka kwenye mwezi ni kilometa 380,000.Lakini umbali mkubwa zaidi ni kilometa 408,000 na huu wa
mbali zaidi unaitwa “apogee”, wakati umbali wake wa karibu zaidi ni
kilometa 357,000 na unaitwa “perigee”.Umbali huu unatofautiana kwa asilimia 15, ambapo kipenyo
cha mwezi pia utaonekana kuwa mkubwa kwa asilimia hiyo 15. Wakati huo
huo, eneo lake linaongezeka kwa asilimilia 30, yaani mara mbili ya
asilimnia15.Kwa hiyo mwezi mpevu wa karibu zaidi utang’aa kwa asilimia
30 zaidi kuliko mwezi mpevu wa mbali zaidi na uso wa dunia, ambao
tunaita kama Mwezi Mpevu (Micro Moon).Kimsingi, mwezi unavutia sana kuuangalia unapochomoza
kwenye upeo wa macho au unapotua katika anga za upeo wa upande wa
magharibi. Huonekana mkubwa na wenye rangi ya dhahabu kwa vile mwanga wa
bluu unakuwa umechujwa na angahewa.Mwezi nusu unaochomoza unavutia sana, utadhani ni bakuli la
dhahabu linalonig’inia mbinguni. Hata mwezi mpevu unapochomoza angani
upande wa mashariki wakati wa machweo huvutia zaidi kutokana na kung’aa
kama sahani kubwa ya njano.Kwa hiyo fikiria jinsi Mwezi Mpevu Ajabu utakavyovutia utapochomoza upeo wa mashariki saa za magharibi leo.
Ingawa umbali wa Mwezi mpevu huu wa leo ni wa karibu zaidi,
miezi ya kabla na baada ya Novemba nayo pia inahesabiwa kama Miezi
Mipevu Ajabu kwa sababu iko ndani ya asilimia 90 ya umbali wa karibu
zaidi kwa Mwezi.Lakini kwa mujibu wa elimu ya kiastronomia, ukomo wa
asilimia 98 hutumika; ndiyo maana mwezi mpevu wa leo (Novemba 14) ni
Mwezi Mpevu Ajabu hasa kwa mwaka 2016.Umbali wa karibu zaidi wa mwezi utakavyoonekana leo utakuwa
saa 11.30 jioni, yaani kiasi ch saa moja kabla ya magharibi ambapo
mwezi mpevu utachomoza kwa madaha katika upeo wa mashariki wakati jua
linazama upande wa magharibi.Kusema kweli, leo itakuwa ni siku ya ajabu na ya kipekee
kwa kizazi hiki. Kwa hiyo tafuta mahali pazuri panapoonekana wazi wa
upeo wa mashariki ili usikose kuuona Mwezi Mpevu Ajabu ambao utakuwa
mwang’avu wa rangi ya njano, ukichomoza wakati wa machweo ili uufurahie
na pia upate cha kujivunia kwa marafiki zako, na kuweza kuwasisimua
watoto wako kwa miaka 18 ijayo hadi Mwezi Mpevu Ajabu, yaani
“perigee-syzygy” utakapoonekana tena mwaka 2034.