Monday, November 14, 2016

Mwezi mkubwa zaidi kuonekana duniani

Mwezi mkubwa zaidi kuonekana duniani




          MWEZI mpevu utakaoonekana leo Novemba 14, siyo tu ni mwezi mpevu ulio karibu zaidi na Dunia mwaka huu, bali pia ni mwezi mpevu ulio karibu zaidi katika karne hii ya 21.Hali ya mwezi mpevu kukaribia zaidi na dunia katika kipindi cha mwaka wowote ndicho kinajulikana kama Mwezi Mpevu Ajabu (Super Moon) na hii kwa sababu unaonekana mkubwa zaidi kuliko ule unaoonekana unapokuwa mbali zaidi kutoka duniani.Kwa jina la kitaalamu Mwezi Mpevu Ajabu huitwa pia perigee-syzygy. Kila mwaka kuna Mwezi Mpevu Ajabu, lakini huu wa leo ni wa ajabu kwa sababu ni wa karibu zaidi katika miaka 67 iliyopita tangu mwaka 1948, na hautakuwa karibu kiasi hiki tena kwa miaka 18 ijayo hadi Novemba 25, 2034.Kitu chochote kikiwa mbali nasi, huonekana kidogo na kikiwa karibu kinaonekana kikubwa. Hali hii hutokea kwa mwezi pia, kwa vile mzingo wa mwezi kuizunguka dunia si duara kamili ila ni umbo la mduaradufu au mduara mithili ya yai.

            Kwa hiyo kila mwezi umbali wake na dunia hubadilika kutoka juu zaidi hadi chini zaidi. Ukubwa wa mwezi tunavyouona kutoka hapa duniani hubadilika kutegemeana na umbali wake kutoka ardhini. Wastani wa umbali kutoka Duniani mpaka kwenye mwezi ni kilometa 380,000.Lakini umbali mkubwa zaidi ni kilometa 408,000 na huu wa mbali zaidi unaitwa “apogee”, wakati umbali wake wa karibu zaidi ni kilometa 357,000 na unaitwa “perigee”.Umbali huu unatofautiana kwa asilimia 15, ambapo kipenyo cha mwezi pia utaonekana kuwa mkubwa kwa asilimia hiyo 15. Wakati huo huo, eneo lake linaongezeka kwa asilimilia 30, yaani mara mbili ya asilimnia15.Kwa hiyo mwezi mpevu wa karibu zaidi utang’aa kwa asilimia 30 zaidi kuliko mwezi mpevu wa mbali zaidi na uso wa dunia, ambao tunaita kama Mwezi Mpevu (Micro Moon).Kimsingi, mwezi unavutia sana kuuangalia unapochomoza kwenye upeo wa macho au unapotua katika anga za upeo wa upande wa magharibi. Huonekana mkubwa na wenye rangi ya dhahabu kwa vile mwanga wa bluu unakuwa umechujwa na angahewa.Mwezi nusu unaochomoza unavutia sana, utadhani ni bakuli la dhahabu linalonig’inia mbinguni. Hata mwezi mpevu unapochomoza angani upande wa mashariki wakati wa machweo huvutia zaidi kutokana na kung’aa kama sahani kubwa ya njano.Kwa hiyo fikiria jinsi Mwezi Mpevu Ajabu utakavyovutia utapochomoza upeo wa mashariki saa za magharibi leo.
            Ingawa umbali wa Mwezi mpevu huu wa leo ni wa karibu zaidi, miezi ya kabla na baada ya Novemba nayo pia inahesabiwa kama Miezi Mipevu Ajabu kwa sababu iko ndani ya asilimia 90 ya umbali wa karibu zaidi kwa Mwezi.Lakini kwa mujibu wa elimu ya kiastronomia, ukomo wa asilimia 98 hutumika; ndiyo maana mwezi mpevu wa leo (Novemba 14) ni Mwezi Mpevu Ajabu hasa kwa mwaka 2016.Umbali wa karibu zaidi wa mwezi utakavyoonekana leo utakuwa saa 11.30 jioni, yaani kiasi ch saa moja kabla ya magharibi ambapo mwezi mpevu utachomoza kwa madaha katika upeo wa mashariki wakati jua linazama upande wa magharibi.Kusema kweli, leo itakuwa ni siku ya ajabu na ya kipekee kwa kizazi hiki. Kwa hiyo tafuta mahali pazuri panapoonekana wazi wa upeo wa mashariki ili usikose kuuona Mwezi Mpevu Ajabu ambao utakuwa mwang’avu wa rangi ya njano, ukichomoza wakati wa machweo ili uufurahie na pia upate cha kujivunia kwa marafiki zako, na kuweza kuwasisimua watoto wako kwa miaka 18 ijayo hadi Mwezi Mpevu Ajabu, yaani “perigee-syzygy” utakapoonekana tena mwaka 2034.

0 comments:

Post a Comment