Tuesday, July 12, 2016

HISTORIA YA WAPARE SEHEMU YA KWANZA





HISTORIA YA WAPARE
            Wapare ni kabila kutoka milima ya Pare, Mkoa wa Kilimanjaro, kaskazini mwa nchi ya Tanzania. Lugha yao ni Kipare (au Chasu).
Wapare wanatokea katika wilaya za Same na Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro, lakini pia wapo katika wilaya ya Moshi sehemu za Chekereni, Himo, Mabungo,Uchira, Moshi mjini, na pia katika wilaya ya Hai sehemu za Rundugai na mto Weruweru. Wapare pia wanaishi katika wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, sehemu za Bumbuli na Mavumo.Lakini kutokana na mahusiano yaliyopanuka hapa nchini,Afrika na dunia nzima kwa ujumla kutokana na suala la utandawazi wapare wametapakaa kote Tanzania kwa shughuli mbalimbali kwa mfano jamii kubwa ya wapare waliohamia mkoa wa Morogoro na kujenga makazi na hali imekuwa katika mikoa yote hapa nchini na kwingineko.
                 Wapare wanasemekana wametoka katika nchi ya Kenya sehemu za Taita, Taveta na Ukamba. Ni kabila la watu wachache lakini wana ushawishi mkubwa katika nyanja za siasa na uchumi wa Tanzania. Wapare ni miongoni mwa makabila ambayo watu wake wamesoma sana. Wapare pia ni kabila la watu wanaopenda haki (yaani hawapendi kuonewa wala kumuonea mtu).Ndio maana watu wengine wanadhani wanapenda kesi,bali kesi ni njia mojawapo ya kuhakikisha haki inatendeka katika jamii.Utawasikia watu wengine wakidai kuwa mpare yupo tayari kuuza ng'ombe kwa kesi ya kuku. Dhuluma kwa Wapare ni kitu kilichokuwa kimepigwa marufuku hata kwenye matambiko yao, japo siku hizi kuna uwezekano baadhi yao wakawa hawana sifa hii tena.
              Wapare walianza kufua chuma kabla ya mwaka 1700 na wafuaji walikuwa wakiitwa Washana, na huo ukoo upo hata leo hii. Wapare walikuwa wakiuza bidhaa zinazotengenezwa na chuma kama majembe,mapanga, visu, silaha kama mikuki kwa makabila ya jirani mfano Wachaga,na wamekuwa na uhusiano tangu siku nyingi. Bidhaa zao hizi ziliuzwa hata kwa Wasambaa (Washambaa).

ITAENDELEA...

0 comments:

Post a Comment