Friday, January 27, 2017

Baadhi ya watumishi Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kuchunguzwa kwa ubadhilifu wa mamilion ya Fedha


Waziri mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka kuwachukulia hatua watumishi Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa waliohusika na upotevu wa fedha za maendeleo ambapo zaidi ya shilingi milioni 700 zilipelekwa katika halmashauri hiyo kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo shilingi milioni 300 za ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri hiyo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Halmashauri alipokuwa katika ziara yake ya Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Pamoja na agizo hilo Waziri Mkuu Majaliwa pia ameuagiza uongozi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU) kuhakikisha inashirikiana katika kufanya uchunguzi ili kubaini watu waliohusika na upotevu huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametahadharisha kuwa Serikali haitowavumilia watumishi wote wanaojihusisha na vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma. Amewataka watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na maadili pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia vizuri fedha za maendeleo zinazopelekwa kwenye maeneo yao na kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Awali akiwa njiani kuelekea Ludewa Mjini akitokea katika kata ya Mundindi Waziri Mkuu alisimamishwa na wananchi wa kijiji cha Mlangali ambao waliiomba Serikali iwasaidie kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ya maji.

0 comments:

Post a Comment