Miezi
saba kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya, kiongozi wa
upinzani Raila Odinga ameituhumu serikali ya Jubilee kwa kuendeleza
ufisadi wa hali ya juu na kupanga njama ya kuiba kura kwenye uchaguzi
huo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mji
mkuu wa Nairobi siku ya Ijumaa, Raila Odinga, kiongozi wa muungano wa
vyama vya upinzani NASA, alidai kuwa serikali ya Uhuru Kenyatta inapora
mali ya umma wakati ambapo anahisi kwamba huenda ikashindwa kwenye
uchaguzi ujao.
"Nilipozungumzia
kashifa ya "NYS" walisema nawaonea wivu juu ya maendeleo wanayofanya,
nilipozingumzia kashifa ya "Eurobond" wakatishia kuniweka kizuizini na
hatimaye hata mkaguzi mkuu wa mahesabu anasema hajaona fedha hizo kwenye
vitabu vya mahesabu katika Benki Kuu,” alisema Odinga.
Kuhusu
zoezi la kusajili wapiga kura ambalo ni la mwisho kabla uchaguzi mkuu
kufanyika, kiongozi huyo wa upinzani alidai kuwa serikali inatumia
maafisa wa utawala kuhimiza usajili katika ngome za jubilee. Raila
alisema maafisa hao hao katika ngome za upinzani wanatishwa dhidi ya
kufanya hivyo.
Viongozi
wa chama tawala cha Jubilee hata hivyo wameyapuuza madai ya Raila. "Ati
anasema kuzunguka kwangu kuomba watu wajiandikishe, ni kuiba kura. Hiyo
siasa ya vitisho tuache, watu wakitaka tushindane, tushindane kwa sera
na yeye awaambie watu ni atawafanyia," alisema Rais Kenyatta katika
mmoja ya mikutano yake.
Hayo
yanaendelea huku zoezi la kusajili wapiga kura ambayo ni awamu ya
mwishi likiingia wiki ya pili sasa. Kila upande unafanya kampeni ya
kushawishi wapiga wananchi katika ngome zao kujisajili kama wapiga kura
huku Tume ya Uchaguzi IEBC ikisema haitaongeza muda wa usajili.
"Hatuoni
tukiongeza muda huu kwa hivyo ikiwa hutajisalili wakati huu hutaweza
kushiriki kwenye uchaguzi,” alisema mkurugenzi wa IEBC Ezra Chiloba.
Tume
ya uchaguzi inalenga kusajili wapigakura wapya wapatao milioni 6
ingawaje kufikia sasa ni takriban wapiga kura milioni moja pekee
waliosajiliwa.
Uchaguzi
mkuu ujao unaelekea kuwa kati ya mafahari wawili, Rais Uhuru Kenyatta wa
Chama cha Jubilee anayetetea kiti chake na mgombea wa muungano mpya wa
upinzani wa National Super Alliance, NASA ambao mgombea wake bado
hajatangazwa. Zaidi ya vyama 15 vya upinzani vimeungana na muungano wa
CORD kubuni muungano mpya wa NASA.
chanzo DW HABARI
0 comments:
Post a Comment